Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria kongamano la wazi kuhusu elimu ya mikopo ya asilimia 10 inayotarajiwa kuanza kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Mpogolo amesema kiasi cha sh. bilioni 14 zimetengwa kwaajili ya mikopo hiyo kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Amesema kongamano hilo linaambata na maonesho ya bidhaa za wajasiriamali, litafanyika Novemba 11 -12 mwaka huu.
“Tutatoa elimu muhimu ya kuhusu mikopo hii tunayotarajia kutoa. Pia elimu ya nishati safi. Hivyo ninawaomba wananchi wake kwa wingi Mnazi Mmoja siku hiyo,” amesema Mpogolo.
Ameeleza, kongamano hilo ni muhimu kwani litatoa elimu ya kutosha kuhusu mikopo hiyo, elimu ya matumizi, urejeshaji na elimu ya nishati safi.
“Nikongamano kubwa na litapambwa na maonyesho na burudani mbalimbali. Wananchi waje kushiriki,” amesema Mpogolo.