Na Mwandishi Wetu - MoHA, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amewakumbusha watanzania wote kubeba jukumu la kushughulika na suala la uzalendo na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana kama ambavyo Mungu alivyoelekeza kufanya hivyo kupitia vitabu vitakatifu.
Waziri Masauni ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa pitio la kitabu cha Uzalendo na Uislam kilichoandaliwa na Mwenyekiti wa MwinyiBaraka Islamic Foundation Sheikh Issa Othman Issa, katika Hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam, tarehe 23 Novemba, 2024.
Aidha Waziri Masauni alisisitiza umuhimu wa Wanazuoni kutoa elimu ya uzalendo ili kuwa na taifa lililo na maadili mema na kuthamini utamaduni wetu "kila mmoja kwa nafasi yake alipo atambue anawajibu na dhamana katika kusimamia suala la maadili, kwani sisi ni wachunga na Mungu atatuuliza juu ya kile tulicho kichunga". Alisema Waziri Masauni.
Vilevile Waziri Masauni amesema Serikali inatambua na kuthamini juhudu za Wanazuoni katika kutunga kitabu hicho na kuendeleza mijadala yenye manufaa kuhusu uzalendo na maadili katika Uisilam, "tumeona umuhimu wa kitabu hiki kwasababu kinaendana na juhudu za Serikali katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kukuza maadili mema miongoni mwa raia" Waziri Masauni aliongeza
Naye Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakary Zubeiry bin Ally, amesema kitabu hicho kimekuja wakati muafaka ambapo kitakuwa msaada hata kwa siku za mbeleni, vilevile amempongeza mtunzi wa kitabu hicho ikiwa ni pamoja kuwasisitiza Wanazuoni na Masheikh kuendelea kutunga vitabu vinavyolenga kuelimisha jamii. "mtu bora ni yule aliye na manufaa kwa watu sambamba na watu kunuifaika na kazi yake, ninyi ni Masheikh lazima muwe na kazi ya kusomesha jamii yetu" Alisisitiza Mufti
Kwa upande wake mtunzi wa kitabu hicho ambaye ni Mwenyekiti wa MwinyiBaraka Islamic Foundation, Sheikh Issa Othman Issa amesema miongoni mwa mambo yaliyo katika kitabu hicho ni pamoja na suala la uzalendo kuwa ni tunu adhimu ambayo inamgusa kila mtu kama raia wa taifa, "katika Uislam uzalendo ni zaidi ya hisia za kawaida ambayo ni sehemu ya maadili yanayokubalika yanayounganisha imani na jukumu la mtu kwa jamii na nchi yake". Alisema Sheikh Issa.
Akizungumza kwa niaba ya Masheikh aliohudhuria mkutano huo, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar amesema kitabu hicho kitakuwa msaada kwani kitasaidia kuwafundisha watu umuhimu wa uzalendo na kujitoa kwaajili ya Nchi.