Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu wakiwasili katika kituo cha afya Bugarama kilichopo halmashauri ya Msalala kwa ajili ya kutoa zawadi ya sikukuu ya krismasi kwa wagonjwa na wauguzi wa kituo hicho. |
Mgodi wa Barrick Bulyanhulu umekabidhi zawadi za Sikukuu ya Krismasi, kwa wazazi na wagonjwa waliolazwa kwenye wodi, katika kituo cha Afya Bugarama, halmashauri ya Msalala, sambamba na Wafanyakazi wa kituo hicho.
Meneja Mkuu wa Mgodi huo Cheick Sangare akiambatana na baadhi ya wafanyakazi walishiriki kugawa zawadi mbalimbali na kwa wafanyakazi wa kituo hicho.
Akizungumza wakati wa hiyo Meneja Mkuu wa Mgodi huo wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare, alisema kampuni itaendelea kushiriki shughuli za maendeleo kwa jamii inayoishi kuzunguka mgodi huo.
Alisema Barrick Bulyanhulu imefanikiwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa zahanati 28 katika Halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga na Halmashauri ya Nyang’hwale, mkoani Geita ambazo zipo zilizokamilika na kuanza kutoa huduma na nyingine zipo katika hatua mbalimbali ya ujenzi.
Alisema sambamba ujenzi huo Mgodi pia umechangia fedha katika utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo katika sekta ya elimu kwa kujenga shule za sekondari katika halmashauri hizo za Msalala na Nyang’hwale na miradi mingine ya sekta za kimkakati ikiwemo maji.
Mgeni rasmi katika fafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Msalala, Charles Fusi aliipongeza mgodi huo kwa kuchangia kuleta maendeleo na kushiriki kusaidia changamoto zinazowakabili wakazi wa maeneo ya jirani “Hili zoezi linalofanyika hapa la kutoa zawadi kwa wagonjwa na watumishi wa kituo cha afya Bugarama ni ishara kubwa jinsi ambavyo mgodi huo, unavyoshirikiana na jamii yetu kwa upendo”. Alisema Fusi.
Alisema katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, jumla ya zahanati 18 zimejengwa katika halmashauri yake na tisa kati yake zimeanza kutoa huduma ya afya kwa wananchi.
“Kwa niaba ya serikali nichukue nafasi hii kuwashukuru wenzetu wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa ushirikiano na kazi nzuri kwa jamii ya Msalala, hasa kwa wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi wa barrack, sisi kama serikali kupitia halmashauri yetu tunawapongeza kwa mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo,” alisema Fusi.
Mganga Mfawidhi, Kituo cha Afya Bugarama, Dk. Silas Kayanda, alisema Mgodi huo kupitia kitengo cha Mahusiano kimekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kituo hicho.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Bugarama, Jesca Msomi alisema Mgodi huo umefanikiwa kutekeleza ujenzi wa shule ya sekondari Ilogi iliyopo katika kata hiyo, kwa asilimia 100 na kwamba Fedha zinazotokana na pato ghafi la uzalishaji wa madini ya dhahabu, (CSR), zimefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya Elimu, Afya na Maji.
Mmoja wa wagonjwa waliopokea zawadi Bi.Elizabert Nicolaus akiongea kwa niaba ya wenzake alitoa shukrani kwa Barrick Bulyanhulu kwa kuwakumbuka katika kipindi hiki cha Sikukuu.