SPIKA DKT. TULIA: WATU WAACHE MAJUNGU TUFANYE KAZI







 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amewataka Wananchi kuacha tabia za kuendekeza majungu na badala yake wajikite katika kujenga taifa.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Disemba 24, 2022 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 kwa Wajumbe wa Mkutano mkuu maalum wa Chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Tughimbe.

Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu wasiopenda maendeleo wanapoona Viongozi wakiwemo wakitaifa wakifanya kazi nzuri kwa jamii wao wanapambana kutengeneza majungu na kukosoa utendaji ili kuleta mkanganyiko usio na faida kwa jamii.

Amewataka Wananchi wakiwemo wa Jimbo hilo kuendelea kumuunga mkono katika majukumu yake ili aweze kuwatimizia mahitaji yao ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, elimu, afya n.k kwa kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Maryprisca Mahundi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ndg. Humphrey Nsomba ambao wamempongeza Dkt. Tulia kwa namna ambavyo ameweza kufanya mabadiliko ya maendeleo ya haraka katika Jimbo hilo kwa kipindi chake kifupi cha Uongozi.