BOA KUANDAA JUKWAA LA KUWAKUTANISHA WAFANYABIASHARA, KUBORESHA HUDUMA ZAKE

 


Na Mwandishishi Wetu

Bank of Africa (BOA), inatarajia kuandaa jukwaa la kuwakutanisha wafanyabiashara wa ndani, kutoa fursa ya kuonyesha bidhaa na huduma zao kati yao katika juhudi za kukuza ushirikiano.

Akizungumza na wateja wa benki hiyo na wadau, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Wasia Mushi, alisema lengo la kuandaa jukwaa hilo la kibiashara na ni kuwaleta pamoja wafanyabiashara kubadilishana uzoefu.

“lengo kuu la jukwaa hilo ni wafanyabiashara kuongeza na kupanua wigo wa biashara zao na kuzileta pamoja na kuzionyesha na kufungua fursa ya biashara na kupanua wigo wa mahusiano na mitandao ya kibiashara,” alisema.

Mushi alisema benki hiyo itaendelea kuandaa makongamano na mafunzo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi, usimamizi wa fedha na huduma zingine za kibenki kuendelea kusogezwa karibu na wateja katika juhudi za kuwarahisisha wateja wao huduma.

Alisema wataboresha na kuendelea kukuza huduma zake za kibenki zikiwemo huduma za uwakala, simu na mifumo yote ya matumizi ya teknolojia (Tehama) katika jitihada za kukuza biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchini.

“benki yetu inatoa ahadi kuendelea kutoa huduma bora na uwajibikaji wa hali juu katika kuhakikisha ustawi wa wateja wetu na kuchochea maendeleo uchumi katika sekta mbalimbali hapa nchini,” alisema.

Mushi alisema wamejipanga kuboresha huduma zake, kuhudumia makundi yote ya wateja kuanzia wateja binafsi, Wafanyabiashara na kampuni  kufanikisha ajenda ya serikali ya kukuza ushirikishwaji wa kifedha.

Pia Mushi alisema ni heshima kwa uongozi wa benki kuandaa futari kwa wateja wa benki hiyo, pamoja na kukuza hisia za jumuiya kati ya imani mbalimbali.

Alisema umuhimu wa kushiriki pamoja kupata Iftar katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na umuhimu wa kuishi pamoja kidini na kuheshimiana kwa ajili ya kudumisha amani, maelewano na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake Sheikh Ramadhan Koba, kutoka Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA),  ameipongeza  BOA kwa kuandaa futari, ambapo katika hadithi za Mtume Muhammad, inaelezwa kwamba “anayemlisha Muumini aliyefunga hulipwa sawa na baraka zote za waliokaribishwa.”