BASHE, MPINA USO KWA USO KISESA

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Kilimo, Husein Bashe atua Kisesa na kukutana na Mbunge wa jimbo hilo, mkoani Simiyu, Luhaga Mpina ana kwa ana na kumtaka kuacha siasa katika zao la Pamba, kwani Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inahitaji kuona fedha zinazotengwa zinanufaisha wakulima.

Bashe amewaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa serikali inarejesha kitalu cha mbegu kuwapatia ruzuku  ya  dawa za wadudu katika zao la mahindi na pembejeo na  mbegu katika zao la Pamba.

“Rais Samia amefanya kazi kubwa katika kilimo Mpina amesema hapa na mimi nataka nisisitize tuweke mambo mengine pembeni aache siasa na sitaki siasa katika zao la Pamba, nafahamu zipo changamoto lakini tulipotoka sio tulipo sitakubali mtu arudishe nyuma jitihada hizi wanaoteseka wananchi,”alisema.

Aidha Bashe amekabidhi trekta 40 kwa jimbo hilo na kuwataka maafisa kilimo na ugani kuacha kukaa mjini na kuishi vijijini ili waweze kuwasaidia wakulima utaalamu na kufikia malengo ya serikali ya kilimo chenye tija.

Pia amewashukuru wazee wa kimila kwa kumsimika kuwa mtemi wa jimbo hilo.

“Nami leo nimesimikwa kuwa mtemi wa Kisesa hivyo Mpina akinitambia pale bungeni kwa kuingia na fimbo ya uchifu nami nitaingia na yangu,”amesema.

Naye Mkuu wa mkoa huo, Kennan Kihongosi amemuhakikishia Waziri Bashe kuwa yeye ndio mwenye dhamana na mkoa huo, hivyo hawezi vumilia watu wanaotafuta umaarufu katika siasa kuingiza masuala ya maendeleo.

“Nimetumwa kazi na Rais Dk. Samia, Simiyu ni ya kwanza ama ya pili katika kuzalisha pamba hivyo kwa wananchi ni zao la kiuchumi sitaki wanasiasa watumie zao hilo kutafuta umaarufu shida zinazosemwa katika zao hilo si za kweli wananchi wa Kisesa msikubali kutumika,”amesema

Naye Mbunge Mpina ametumia fursa hiyo kumkaribisha Bashe Kisesa na kueleza kuwa wanazo tofauti zao hali iliyowafikisha hadi Mahakamani lakini yupo tayari kushirikiana naye katika masuala ya utendaji wa serikali.