WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema marathon zinazofanyika kila kona nchini ni mpango mkakati wa kuwafanya Watanzania wawe na afya njema na wakae pamoja ili kubadilishana mawazo.
“Ni mkakati wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwahamasisha wananchi wetu kufanya mazoezi ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari na presha,” amesema.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 14, 2024) wakati akizungumza na viongozi na wadau mbalimbali walioshiriki Ruangwa Marathon 2024 (Msimu wa Pili) katika viwanja vya Madini, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Mbio hizi za Ruangwa ni zaidi ya mbio kwa sababu malengo yake makubwa ni kuhamasisha wana-Ruangwa tuwe na umoja; tuimarishe ujenzi wa afya zetu, tupate fursa ya kufahamiana na kuimarisha urafiki,” amesema.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa, amewataka Wana-Ruangwa wajitokeze kusimamia miradi ya maendeleo iliyomo kwenye wilaya hiyo na kupitia mkusanyiko mkubwa kama huo watengeneze mijadala ya kiuchumi katika ngazi na makundi tofauti waliyopo.
Amewashukuru washiriki wa mbio hizo za km.21, km.10, km.5 na km.3 kwa watoto kutoka Ruangwa na wilaya za jirani za Nachingwea na Liwale lakini pia vikundi vya hamasa na marathon kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Iringa na Mtwara.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alisema watu wanashauriwa kufanya mazoezi ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza na endapo watafuata hayo maelekezo, Serikali itaokoa fedha nyingi zinazotumika kutibu magonjwa hayo.
“Nchi yetu inapoteza sh. bilioni 454 kwa mwaka kwa kutibu watu wenye magonjwa ambayo tukifanya mazoezi tu, nchi yetu inakuwa salama. Fedha hizi zingetumika kujenga shule za msingi mpya 1,513 zenye madarasa nane na ofisi za walimu,” alisema.
Mapema, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alisema Ruangwa Marathon inaelekea kuwa ya Kimataifa katika miaka michache ijayo. Alimpongeza Mbunge wa Ruangwa kwa kuandaa marathon hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye, msanii wa Bongo Fleva nchini, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga miradi ya maendeleo wilayani Ruangwa ikiwemo barabara ya lami ya kutoka Nanganga.
“Mwaka jana tulikuja kufanya tamasha na njia nzima ilikuwa rough sana, nikawa najiuliza kama tungeweza kurudi salama tulikotoka. Lakini mwaka huu, nimeshangaa sana. Tumekuja kwenye lami tangu njiapanda. Leo hapa Ruangwa, tutazindua tamasha la mwaka huu la Wasafi Festival na kisha tutaendelea na mikoa mingine,” alisema.