DK. TULIA ASISITIZA UMUHIMU WA VIJANA KUPEWA KIPAUMBELE CHA ELIMU NA AJIRA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa vijana wengi duniani wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo elimu duni na ukosefu wa ajira, hali inayowasababisha kukosa matumaini, kujiingiza katika uhalifu, kuandamana mitaani na kuhama nchi zao kwa kutafuta maisha bora.

Amesisitiza kuwa, katika nyakati hizi zenye misukosuko duniani mahitaji ya vijana hayapaswi kupuuzwa. Amehimiza Viongozi na Wabunge kuhakikisha wanatengeneza mazingira rafiki kwa vijana na kuwapa kipaumbele katika kupata elimu bora na fursa za ajira.

Dkt. Tulia ametoa kauli hiyo leo tarehe 12 Septemba, 2024 wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 10 wa Wabunge Vijana wa IPU unaofanyika Jijini Yerevan, nchini Armenia na kuhudhuriwa na Viongozi wa Mabunge na Wabunge vijana kutoka nchi wanachama wa IPU.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Armenia, Mhe. Nikol Pashinyan.