Na MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM , amesema mvua na jua havitawazuia kumuunga mkono Raia Dk.Samia Suluhu Hassan katika kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Abdallah ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wananchi wa Kata ya Kipumbwi iliyopo Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga, huku mvua kubwa ikinyesha.
"Ndugu wananchi, iwe mvua, iwe jua, tutaendelea, kumuunga mkono Rais Dk.Samia kwa maagizo yake ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kuhakikisha tunatatua changamoto za wananchi wapate huduma bora na maendeleo,"alisema.
Katika siku ya tatu ya ziara, Mwenyekiti Abdallah alifungua mashina matano akiwa njiani kuelekea Kipumbwi Pangani na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Zahanati ya Mikingunj aliyoichangia sh.milioni 25 huku mbunge wa Jimbo hilo akichangia saruji na sh.milioni 4 za mafundi.