Balozi Mbelwa awatahadharisha wafanyabiashara wanaoagiza malori yaliyotumika kutoka Uingereza kuwa makini na kampuni wanazoagizia

Na MWANDISHI WETU

BALOZI wa Tanzania Nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki amewatahadharisha Watanzania wanaoagiza  magari ya usafirshaji Malori yaliyotumika (used), kutoka nchini humo, kuwa makini na kampuni wanazoagizia magari hayo ya kubeba mizigo, kuepuka hasara na usumbufu unaoweza kujitokeza kama ambavyo imetokea hivi karibuni kwa baadhi ya wafanyabiashara wa usafirishaji.

Pia, aliwataka wafanyabiashara  hao wanaoagiza Malori yaliyotumika kuhakiki makampuni wanayoagiza kama yako hai(active), yamesajiliwa na serikali ya nchi hiyo, kupitia tovuti ya nchi hiyo jambo ambalo linafanyika mtandaoni bila malipo yoyote.

Balozi Mbelwa ametoa tahadhari hiyo, jana, baada ya kutoa taarifa ya ufafanuzi juu ya malalamiko aliyoyapata kutoka kwa wafanyabiashara wa hapa nchini,  walioagiza magari hayo  Wingereza pasipo kupatiwa ndani ya kipindi cha miezi sita jambo liliowapa hasara.

"Hivi karibuni Ubalozi, tumepokea malalamiko kutoka kwa Watanzania walioagiza malori hapa Wingereza, baada ya kulipa fedha ndani ya kipindi cha miezi sita pasipo kupata magari yao.Na wengine wametumiwa malori yaliyo chini ya kiwango nje ya makubaliano," alieleza.

Kwa hali hiyo, Balozi Kairuki, aliwashauri  wafanyabiashara wa usafirishaji wanaoagiza magari hayo, kuingia mikataba na makampuni wanayoagiza magari hayo ambapo wanaweza kuwatumia Watanzania(wanadiasplra) wanasheria wanaoishi Uingereza wenye uwezo wa kuandaa mikataba ya manunuzi kwani itawawia wepesi wa kufuatilia mikataba hiyo pale inapojitokeza changamoto kwa kuwa wapo nchi hiyo tofauti na wanunuzi walioko Tanzania.

Alieleza, hali hiyo imeibua usumbufu mkubwa na hasara kwa wafanyabiashara, kwani baadhi yao walikopa mikopo benki na muda wa marejesho umefika kipindi wao hawajapata malori waliyoyaagiza Uingereza.

Balozi Kairuki alitaja sababu za  wafanyabiashara wa usafirishaji wengi kutoka Tanzania kupenda kununua Malori hayo yaliyotumika kutoka Nchini Uingereza ni uimara wa magari hayo, gharama nafuu kulinganisha na mataifa mengine, kiti cha dereva kuwa mkono wa kulia.

Katika hatua nyingine, Balozi Kairuki alisema  ubalozi unaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo na wote walio wasilisha malalamiko hayo kufahamu kampuni walizoagizia na kupata ufumbuzi wa jambo hilo.