BILIONI 3.9 KUIMARISHA MIUNDOMBINU HIFADHI YA TAIFA IBANDA-KYERWA


Na MWANDISHI WETU

Serikali imetoa sh. Billioni 3.9 ya kuimarisha miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyerwa iliyoko mkoani, Kagera, jambo ambalo litachochea ongezeko la watalii na kukuza uchumi.

Akikagua miradi ya ujenzi wa miundombinu hiyo Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Kuji alisema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imewapa  upendeleo wa fedha za kujenga lango la kuingilia watalii (Complex gate), na Nyumba za kisasa za Watumishi eneo la Kifurusa hii yote kuhakikisha tunapata mazingira mazuri ya kufanyia kazi zetu.

“Hili ni deni ambalo Mhe.Rais wetu ametupa sisi TANAPA na hususani watumishi wa Hifadhi hii na tutamlipa kwa kuchapa kazi na kujituma zaidi katika kulinda na kutunza Rasilimali hizi kwa faida ya kizazi cha sasa na kile cha baadae” alisema Kamishna Kuji.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick Mofulu, ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyerwa, alisema ujenzi wa lango hilo la Hifadhi unahusisha sehemu ya ukaguzi wa nyaraka na malipo, ofisi za wahasibu, ofisi za askari upande wa kuingia na kutokea, ofisi ya Afisa Utalii na msaidizi wake, ofisi ya Tehama, ujenzi wa barabara kilometa mbili, na mifumo ya umeme.

Pia, ujenzi wa vyoo upande wa kuingia, na kutokea vyenye mashimo 7 ya kawaida 1 walemavu kwa kila jengo, uchimbaji wa visima viwili, fensi ya umeme mita 400, Nyumba 2 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 2), Nyumba 3 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 4), vimbweta 08, sehemu ya kupaki magari makubwa na madogo upande wa kutoka na kuingia lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5400, mfumo wa umeme jua, pamoja na eneo la kupumzikia wageni. 

Kazi ambayo inatekelezwa na Kampuni ya MJT Crew Co. Ltd na JV Sumry’s Enterprises Ltd za hapa nchini ambapo mpaka sasa ujenzi uko asilimia 55 na inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.