MUHIMBILI SASA KUPANDIKIZA MIMBA, DK.MPANGO AZINDUA JENGO LA KISASA

MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango, amezindua jengo maalumu la upandikizaji wa mimba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ikiweka historia ya kuwa Taasisi ya kwanza ya serikali  kutoa huduma hiyo ya kibingwa, ambayo itakuwa msaada mkubwa nchini kuondoa changamoto ya uzazi na kuepusha wananchi kuifuata nje ya nchi.

Pia, Dk.Mpango, akizindua mpango wa upapandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa watoto 14 hospitalini hapo na uzinduzi wa gari la Matibabu linalotembea (Mobile Medical Service) ikiwa ni hatua kubwa ya kuchochea utalii tiba nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam,  alipokuwa akizindua huduma hizo Muhimbili,  Dk.Mpango amesema uzinduzi wa huduma hizo za kibingwa nchini ni mwendelezo wa dhamira ya serikali ya kuwa na Taifa bora lenye wananchi wenye afya imara watakaoleta maendeleo.

"Hatua hii  ni maendeleo makubwa kwani ni huduma mpya katika Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili na taasisi za serikali nchini ikiwa ni azma ya serikali ya Rais Dk.Samia  Suruhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kibobezi nchini ambazo awali walikuwa wakizifuata nje ya nchi," amesema.

Amesema huduma hizo ni muhimu na faraja kwa upandikizaji wa mimba kuanza kufanyika nchini ikiwa ni mara ya kwanza kwa  kituo cha serikali kuanza kutoa huduma hizo muhimu kuondoa changamoto zilizopo katika jamii.