THRDC YAGUSWA NA KAULI NZURI YA NCHIMBI, YAJIPANGA KUKUTANA TENA NA RAIS SAMIA KUJADILI HAKI ZA BINADAMU

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema umeguswa na kufurahishwa na kauli nzuri zilizotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi za kupinga vitendo vya utekaji nchini vilivyozua hofu na kutaka serikali kulipatia ufumbuzi haraka suala hilo.

THRDC umesisitiza kuwa viongozi wote wakitoa kauli kama Dk. Nchimbi itakuwa rahisi kufikia lengo la kutokomeza magenge ya utekaji nchini. 

Hayo yamesemwa na Mratibu wa THRDC,   Wakili Onesmo Ole Ngurumwa alipozungumza na Uhuru jioni ya leo.  Amesema kauli za Dk.Nchimbi zimeleta faraja zikionyesha mshikamano wa CCM na vyama vingine na wadau mbalimbali kupinga vitendo hivyo viovu vya utekaji na ukiukwaji wa haki za watu. 

Katika hatua nyingine, Wakili Ole Ngurumwa akizungumzia maazimio ya Mkutano Mkuu w 13 wa THRDC uliofanyika Septemba, 12, mwaka huu, jijini Arusha akisema  katika mkutano wao  huo walifanya tathmini ya hali ya haki za binadamu ilivyo sasa, huku wakiazimia, kukutana na Rais Dk. Samia kuzungumza naye  suala hilo na kuhimiza uimarishaji  wa haki za binadamu nchini ambayo imekuwa akiifanya  toka aingie madarakani.

Amesema  wanarudi kwake kwa kuwa alituahidi  tukiwa na jambo zito la kushauri na kujadililiana milango yake ipo wazi, alisema hayo wakati aliposhiriki Mkutano Mkuu wa 10 wa THRDC  uliofanyika mwaka 2022.

Ameeleza, katika kutambua mchango na nafasi ya Rais Dk. Samia katika kutatua changamoto za  haki za binadamu nchini, wanatarajia kukutana naye muda wowote kuanzia sasa pindi atakapokuwa tayari, kuzungumza naye na kutoa maoni yao mbalimbali juu ya masuala uimarishaji wa haki za binadamu nchini kama anavyosisitiza kupitia falsafa yake ya  4R ambayo imewaunganisha Watanzania. 

Amesisitiza kuwa, Rais kwa mujibu wa katiba ndiyo mwenye dhamana ya kulinda haki za binadamu na usalama wa raia wake, hivyo kwenda kwake ni tunadhani tunakwenda sehemu sahihi.