Na MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mary Maganga ameuagiza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kuhakikisha inazingatia ubora wa huduma inazotoa kwa wananchi kuendana na ithibati ya utoaji wa huduma kwa viwango vya kimataifa, waliyopata.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam katika hafla ya WCF, ya kukabidhiwa Cheti cha Ithibati ya utoaji wa huduma bora kwa viwango vya kimataifa (ISO certification).
Akikabidhi cheti hicho kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk. John Mduma, Maganga alisisitiza kuwa maboresho yanayofanywa na Mfuko huo yanapaswa kuzingatia mahitaji na matarajio ya wateja wake kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa haki yao ya fidia stahiki pale wanapopatwa na madhila yatokanayo na kazi zao.
“Kitu cha msingi ni kuhakikisha mnaendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma zenu. Nasisitiza mtumie ithibati hii mliyoipata kurahisisha taratibu za kuwasajili waajiri ikiwezekana waweze kujisajili wenyewe kwa hiari badala ya kulazimishwa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria,” amesema Bi. Maganga.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa jitihada za kutoa elimu kwa wadau wake pamoja na kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali ili kuhakikisha huduma zake zinakidhi mahitaji ya wateja ni muhimu kuzingatiwa.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amebainisha kuwa mafanikio waliyoyapata yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mkubwa wanaofanya katika matumizi ya mifumo ya Tehama.